Sunday, 27 April 2014

ZICHANE BILA MAUMIVU… JUA LEO!

Huu ni muongozo juu ya kutunza na kuchana nywele asilia bila maumivu au ugumu wowote.
  • Kabla ya kuendelea kusoma; amini kuwa nywele asilia ni rahisi kutunzwa; Unachotakiwa kujua ni JINSI GANI hutunzwa.
  • Pia tambua kuwa; kutokuwepo na masaluni au makala mengi juu ya utunzaji wa nywele asilia hakumaanishi kuwa kuna ugumu katika kutunza nywele hizi bali tu ni uhaba wa watafiti, na unaweza kuwa moja wao. 
  • Nywele zetu ni tofauti na zile za asili ya kizungu, hivyo njia za matunzo na mitindo sio lazima zifanane.

Haya tuendelee; kama nywele nyinginezo, matunzo ya nywele asilia huusisha usafi, michano na mitindo.

1) USAFI 

  • Kwa kutumia shampoo osha nywele zako walau mara moja kwa wiki hata zaidi kama kuna ulazima wa kuondoa mafuta, jasho, vumbi nk. Nywele zenye afya hukua katika mazingira safi. 
  • Kwa kawaida shampoo hukakamaza nywele, hivyo hakikisha watumia kondishina wakati wa kuziosha. Hii hulainisha nywele  na kuzifanya rahisi kuchanwa. 
  • Fanyia stimingi nywele zako mara moja kwa wiki. Kama utainigia katika stima; vaa kofia ya plastiki kabla ya kufanya hivyo kwani joto kali huletea nywele madhara.
  • Wakati wote tumia vidole vyako badala ya kucha kusugua na kumasaji ngozi ya kichwa chako.

TAMBUA: Kuosha nywele hakufupishi nywele kama inavyoaminika; ila tu hurudisha nywele katika asili yake ya kujiviringisha, hivyo achana na imani hii; weka nywele zako safi kwa afya ya nywele zako.

2) JINSI YA KUCHANA NYWELE ASILIA

Inaaminika kuwa nywele asilia ni ngumu na huuma wakati wa kuchanwa; SIO KWELI, ila tu wengi wetu hatujui njia fasaha ya kuchana nywele zetu.

Kabla ya kuendelea, tutambue kuwa kuchana mara kwa mara nywele asilia katika hali ya ukavu hukata nywele.  Hii hutokana na  msuguano pamoja na nguvu itumikayo katika kuvuta nywele iliyojifungafunga wakati wa uchanaji .

Jambo hili hufanya nywele zionekane kama hazirefuki. Ukweli ni kwamba nywele hurefuka muda wote, sema tu mabadiliko hayo hayaonekani kwasababu spidi ya kukatika ni kubwa kuliko ile ya  kurefuka kwa nywele.

NYWELE ASILIA HUCHANWA KATIKA HATUA ZIFUATAZO.

  1. Baada ya kuosha , stimingi nk. Kausha nywele zako kidogo tu kwa kukandamiza taulo juu ya nywele zako kwa sekunde chache. Usikaushe nywele zako kwa kuzipangusa, kwani msuguano kati ya nywele na taulo lako husababisha nywele kukatika .  
  2. Katika nywele zenye unyevu;  paka mafuta yako ya asili (mf zeituni, nazi, jojoba nk) kwenye ngozi.  Mafuta katika hali ya kimiminika ni rahisi kusambaa kama yanapatikana. 
  3. Baada ya hapo sambaza kiasi fulani cha mafuta hayo kwenye kiganja chako kisha yapake juu ya nywele na kwenye ncha zake. Masaji kichwa chako ili kuyasmabaza. 
  4. Kwa kutumia CHANUO LENYE MENO MAKUBWA; anza kuchana nywele zako kuanzia kwenye ncha zake kushuka kwenye ngozi. Kumbuka  kuanza kuchana nywele kuanzia kwenye ngozi kuelekea kwenye ncha  husababisha maumivu makali na hukata nywele kama ncha hizi zimefungamana. 
  5. Baada ya hatua ya 4, ziache nywele zako zikauke kwa hewa. Lakini pia waweza ku-blow-dry nywele zako kuanzia kwenye ncha kuelekea kwenye ngozi; ila tambua kuwa matumizi ya mara kwa mara ya moto huletea nywele madhara.


KUMBUKA: Kila kabla ya kuchana nywele zako , spreyi kiasi fulani cha maji juu ya nywele zako kisha zipake ncha zake kiasi fulani cha mafuta.

Maji na mafuta hulainisha na kuachanisha ncha zilizojifunga hivyo kuwezesha nywele zako kuchanika kirahisi bila maumivu yoyote.

3) MITINDO
  • Furahia mitindo unayoipenda; ila tambua kuwa mitindo salama ni ile isiyokata nywele na hatari ni ile ikatayo nywele. 
  • Ukiona mtindo Fulani unakukatia nywele usijipe moyo; achana nao mara moja, lasivyo utapoteza kiasi kingi cha nywele. 
  • Nywele zenye aftya na zisizokatika hazibaki kwa wingi kwenye chanuo wala bafuni wakati wa kuoshwa. Ukiona hali tofauti na hii jua kwamba kuna tatizo na nywele zako linatotakiwa suluhisho la haraka. 
  • Mfano wa  mtindo hatarishi ni rasta ndogo sana za vitunguu. Mingineyo mingi pia ipo.

                       Tunakutakia makuzi mema ya nywele zako :)



 Kwa maswali na ndondoo zaidi, endelea kufuatilia ukurasa wetu SIRI YA UREMBO pamoja kufanya 
utafiti binafsi.  Wasambazie na warembo wengine.

1 comment:

  1. Asante ndugu kwa maelezo ya kina. Natumai wengi tutanufaika iwapo tutabahatika kusoma maelezo hayo kwa usahihi.

    ReplyDelete