Huu ni muongozo juu ya kutunza na kuchana nywele asilia bila maumivu au ugumu wowote.
- Kabla ya kuendelea kusoma; amini kuwa nywele asilia ni
rahisi kutunzwa; Unachotakiwa kujua ni JINSI GANI hutunzwa.
- Pia tambua kuwa; kutokuwepo na masaluni au makala
mengi juu ya utunzaji wa nywele asilia hakumaanishi kuwa kuna ugumu katika
kutunza nywele hizi bali tu ni uhaba wa watafiti, na unaweza kuwa moja wao.
- Nywele zetu ni tofauti na zile za asili ya kizungu,
hivyo njia za matunzo na mitindo sio lazima zifanane.
Haya tuendelee; kama nywele nyinginezo, matunzo ya
nywele asilia huusisha usafi, michano na mitindo.
1) USAFI
- Kwa kutumia shampoo osha nywele zako walau mara moja
kwa wiki hata zaidi kama kuna ulazima wa kuondoa mafuta, jasho, vumbi nk. Nywele
zenye afya hukua katika mazingira safi.
- Kwa kawaida shampoo hukakamaza nywele, hivyo hakikisha
watumia kondishina wakati wa kuziosha. Hii hulainisha nywele na kuzifanya rahisi kuchanwa.
- Fanyia stimingi nywele zako mara moja kwa wiki. Kama utainigia
katika stima; vaa kofia ya plastiki kabla ya kufanya hivyo kwani joto kali
huletea nywele madhara.
- Wakati wote tumia vidole vyako badala ya kucha kusugua
na kumasaji ngozi ya kichwa chako.
TAMBUA: Kuosha nywele hakufupishi nywele kama
inavyoaminika; ila tu hurudisha nywele katika asili yake ya kujiviringisha,
hivyo achana na imani hii; weka nywele zako safi kwa afya ya nywele zako.
2) JINSI YA KUCHANA NYWELE ASILIA
Inaaminika kuwa nywele
asilia ni ngumu na huuma wakati wa kuchanwa; SIO KWELI, ila tu wengi wetu
hatujui njia fasaha ya kuchana nywele zetu.
Kabla ya kuendelea, tutambue kuwa kuchana mara kwa
mara nywele asilia katika hali ya ukavu hukata nywele. Hii hutokana na msuguano pamoja na nguvu itumikayo katika kuvuta nywele iliyojifungafunga wakati wa uchanaji .
Jambo hili hufanya nywele zionekane kama hazirefuki. Ukweli
ni kwamba nywele hurefuka muda wote, sema tu mabadiliko hayo hayaonekani kwasababu
spidi ya kukatika ni kubwa kuliko ile ya kurefuka kwa nywele.
NYWELE
ASILIA HUCHANWA KATIKA HATUA ZIFUATAZO.
- Baada ya kuosha , stimingi nk. Kausha nywele zako kidogo
tu kwa kukandamiza taulo juu ya nywele zako kwa sekunde chache. Usikaushe
nywele zako kwa kuzipangusa, kwani msuguano kati ya nywele na taulo lako
husababisha nywele kukatika .
- Katika nywele zenye unyevu; paka mafuta yako ya asili (mf zeituni, nazi,
jojoba nk) kwenye ngozi. Mafuta katika
hali ya kimiminika ni rahisi kusambaa kama yanapatikana.
- Baada ya hapo sambaza kiasi fulani cha mafuta hayo
kwenye kiganja chako kisha yapake juu ya nywele na kwenye ncha zake. Masaji kichwa
chako ili kuyasmabaza.
- Kwa kutumia CHANUO LENYE MENO MAKUBWA; anza kuchana
nywele zako kuanzia kwenye ncha zake kushuka kwenye ngozi. Kumbuka kuanza kuchana nywele kuanzia kwenye ngozi
kuelekea kwenye ncha husababisha maumivu
makali na hukata nywele kama ncha hizi zimefungamana.
- Baada ya hatua ya 4, ziache nywele zako zikauke kwa
hewa. Lakini pia waweza ku-blow-dry nywele zako kuanzia kwenye ncha kuelekea
kwenye ngozi; ila tambua kuwa matumizi ya mara kwa mara ya moto huletea nywele madhara.
KUMBUKA: Kila kabla ya kuchana nywele zako , spreyi
kiasi fulani cha maji juu ya nywele zako kisha zipake ncha zake kiasi fulani cha
mafuta.
Maji na mafuta hulainisha na kuachanisha ncha
zilizojifunga hivyo kuwezesha nywele zako kuchanika kirahisi bila maumivu
yoyote.
3) MITINDO
- Furahia mitindo unayoipenda; ila tambua kuwa mitindo
salama ni ile isiyokata nywele na hatari ni ile ikatayo nywele.
- Ukiona mtindo Fulani unakukatia nywele usijipe moyo;
achana nao mara moja, lasivyo utapoteza kiasi kingi cha nywele.
- Nywele zenye aftya na zisizokatika hazibaki kwa wingi kwenye
chanuo wala bafuni wakati wa kuoshwa. Ukiona hali tofauti na hii jua kwamba
kuna tatizo na nywele zako linatotakiwa suluhisho la haraka.
- Mfano wa mtindo
hatarishi ni rasta ndogo sana za vitunguu. Mingineyo mingi pia ipo.
Tunakutakia makuzi mema ya nywele zako :)
Kwa maswali na ndondoo zaidi, endelea kufuatilia ukurasa wetu
SIRI YA UREMBO pamoja kufanya
utafiti binafsi. Wasambazie na warembo wengine.